Event Date: 
22-12-2022

Usharika wa Kanisa Kuu la Azania Front, kwa mara ya kwanza katika historia, uliandaa safari ya kiimani na maombi katika nchi za Misri na Israel. Ziara hiyo ilifanyika kuanzia tarehe 6 hadi 16 Novemba 2022.

Ziara hiyo iliongozwa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa Kuu Chaplain Charles Mzinga.

Ziara hii ilihusisha watu 85 ambapo baadhi yao walitoka Usharika wa Azania Front lakini pia nje ya usharika kama vile sharika za Msasani, Ununio, Mbagala nk. Pia baadhi ya watu walitoka madhehebu mengine nje ya KKKT kama Kanisa Katoliki, Sabato, na makanisa mengine ya kipentekoste. Baadhi walitoka mikoani kama Arusha, Morogoro, Kilimanjaro nk.

Ziara hii ilikuwa ya baraka nyingi kwani kulikuwa na watumishi wengi wa kiroho walioungana na kusaidiana na Chaplain Mzinga katika maombi ya kibinafsi na ya kiujumla yaliyofanyika sehemu mbalimbali tulizotembelea. Watumishi hao ni pamoja na Mchungaji Wilbroad Mastai wa Usharika wa KKKT Kimara, Mchungaji mstaafu Dawson Chao wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Danton Rodrick na Mchungaji Daniel Lema wa Power of God Fire Church, Nabii Nick Shaboka na Mchungaji Rose Shaboka wa New Day Church International pamoja na walimu wa neno la Mungu, wazee wa kanisa na watumishi wengine.

Neno Kuu la ziara hiyo lilitoka katika kitabu cha 2 Mambo ya Nyakati 6:32. “Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israel, atakapokuja kutoka katika nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako kuu, na mkono wako ulio hodari, na mkono wako ulionyooshwa, hao watakapokuja na kuomba wakielekea nyumba hii.”

Ziara hiyo ilianzia nchini Misri ambako tulipata kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria ya Biblia kama Kanisa linaloning’inia (the Hanging Church), Kanisa la Mtakatifu Simon lililo kwenye mapango au mahandaki na lina uwezo wa kuchukua watu 2500 kwa wakati mmoja.

Tulitembelea pia Kanisa la Familia Takatifu (The Holy Family Church) mahali ambapo Yusufu, Maria na mtoto Yesu walikaa hapo miezi mitatu walipomkimbia Herode alipotaka kumuua mtoto Yesu. Watu pia walitembea hadi kilele cha mlima Sinai mahali ambapo Musa alikaa na kufunga kwa siku arobaini. Mlima huo ni mgumu sana kuupanda japo ni kilomita 7 tu. Wengi walifika kileleni na kuona pango ambalo Musa alikaa na kufunga kwa siku arobaini. Tulipata pia nafasi ya kutembelea maeneo mengine yasiyo ya kiimani kama mapiramidi walikozikwa wafalme na pia kwenye manukato yanayotokana na mimea na pia mahali ambapo palitengenezwa karatasi za mwanzo kabisa kutumika katika historia ya mwanadamu (papyrus) ambazo maandishi au michoro yake inadumu hadi miaka zaidi ya 500.

Safari hiyo ilitupeleka hadi Israel ambako tulitembelea maeneo mengi tofauti tukianzia na Boaz Field mahali ambapo wachungaji wa makondeni waliona nyota ya mashariki iliyowapeleka hadi Bethlehemu alikozaliwa mtoto Yesu. Kabla ya kwenda Bethlehemu, tulipita mlima Sayuni mahali ambapo Bwana Yesu aliandaliwa karamu ya mwisho kabla ya kutiwa mikononi mwa watesi wake.

Tulipata pia kuelezwa kuwa Israel ni kitovu cha dunia na Yerusalem ni kitovu cha Israel. Mfalme Daudi alichagua mji wa Yerusalemu kuwa mji mkuu (Mji wa Daudi) kwa sababu kuu nne. Kwanza, kulikuwa na maji  na zabibu na mizeituni hivyo watu hawatakosa chakula na hata wageni hawatalala njaa. Pili ni mahali palipokuwa rahisi kujenga ulinzi na mazingira. Tatu ni mahali pa barabara kuu ambapo hata mababa wa Imani walipita njia hiyo. Nne, Yerusalemu ilikuwa ni eneo jipya ambako hapakuhusiana na Benjamini wala Yuda.

Tulitembelea Kanisa la Mtakatifu Peter la Gallicantu (Church of St Peter in Gallicantu aka Church of St Peter Kokoliko) mahali ambapo ilikuwepo nyumba ya Kayafa alikopelekwa Yesu baada ya kukamatwa kwenye Mlima wa Mizeituni. Hapo pia tuliona gereza alilowekwa Yesu pamoja na wafungwa wengine kama Baraba. Gereza hilo liko chini ya nyumba ya Kayafa kwenye handaki ambako mfungwa anapelekwa akiwa amefungwa kamba miguuni na kutangulizwa kichwa chini.

Pia tulitembelea Bustani ya Kaburi (The Garden Tomb) mahali panaposadikiwa kuwa Bwana wetu Yesu Kristo alizikwa. Maeneo mengi tuliyotembelea ni halisi ambako Bwana Yesu Kristo alipita au alifanya kazi. Bustani ya Kaburi si eneo halisi lakini inasadikika kwamba Bwana wetu Yesu Kristo alizikwa eneo hilo. Hii ni kutokana na ugunduzi wa mwingereza mmoja mwaka 1866 aliyefanya utafiti na kugundua kuwa eneo hilo kuna mawe na yana sura ya fuvu la kichwa. Pia aliona kaburi la kiyahudi moja tu (Kaburi la Yusufu Arimathayo) na pia bustani kwani kulikuwa na chombo cha kukamua mizeituni. Biblia inasema eneo alilosulubiwa Yesu lilikuwa na bustani na kaburi ambalo halijatumika. Kwa mazingira hayo ikasadikika kwamba Yesu alizikwa eneo hilo. Kwa utaratibu wa miaka hiyo watu wenye makosa walisulubiwa nje ya mji na kama hakufa alipigwa mawe. Yesu pia alisulubiwa nje ya mji njiani na ndiyo maana habari zake zilienea kwa haraka kwa sababu ilikuwa njia kuu ya kwenda Damascus, Lebanon hadi Misri.

Tulitembelea Ukuta wa Magharibi (Western Wall) ambapo watu waliweka maombi yao kwenye nyufa za ukuta na kufanya maombi. Ukuta huu pia huitwa Ukuta wa Maombolezo. Nyuma ya ukuta huo ni Mlima Moria mahali ambapo Abraham alitaka kumchinja mwanawe Isaka. Lakini pia ni mahali ambapo mfalme Suleimani alijenga hekalu ambalo lilibomolewa na Mfalme Titus mwaka wa 70 baada ya Kristo na miaka michache baadaye pakajengwa msikiti mkubwa unaoitwa Rock of the Dome ambao umeezekwa kwa paa la dhahabu. Mahali hapa Ukuta wa Magharibi (Ukuta wa Maombolezo), Wayahudi toka pande zote za dunia pamoja na watu wengine hufika pale na kuomba (2 Nyakati 6:32). Watu mashuhuri kama Rais mstaafu Donald Trump wa Marekani na Papa wamewahi kufika. Wayahudi wanaomba kwa matumaini kwamba ipo siku hekalu lile lililobomolewa litakuja kujengwa na wao kurudi kuabudu kwenye hekalu. Wayahudi wanasali hapo masaa 24. Ikumbukwe kwamba toka hekalu hilo lilivyobomolewa, Wayahudi hawana hekalu tena bali masinagogi. Hapo ni mahali ambapo Yesu aliulilia mji kama ilivyo kwenye Luka 19:41-44.

Tulipita pia Bustani ya Getsemane mahali ambapo Yesu alikesha akiomba ili kikombe kimuepuke. Bustani bado ipo na pia kuna Kanisa hapo lililojengwa na mataifa 12 yaani Church of All Nations.

Tulipita pia katika mji wa Yeriko uliokuwa na ukuta imara usioingilika. Hapo Yeriko tuliweza kuona mti aliopanda Zakayo ili apate kumwona Yesu. Yeriko pia tulipanda kwenda mlima wa majaribu na kuona pango ambalo Bwana Yesu Kristo alikaa kwa siku arobaini baada ya ubatizo na kujaribiwa na shetani. Hapo pia tuliona mapango ambayo watawa waliokimbia unajisi mijini walikwenda kujificha na kusali. Walichimba mahandaki mengi na baadaye wakajenga nyumba ya watawa (monastery of temptation) huko mlimani. Kufika huko ilibidi tupande vigari vya angani. Tulitembelea bahari mfu (dead sea) ambayo iko mita 420 chini ya usawa wa bahari na ina kiwango cha juu cha chumvi kinachofikia asilimia 30 na mtu anaweza kuelea akiogelea.

Pia tulitembelea mahali ambapo Nahmani alitumbukia mara saba na kupona magonjwa yake. Huko Yeriko pia tulipita na kuona kisima kile ambacho kilisababisha watu kuzaa mapooza na Elisha akaweka chumvi na shida hiyo ikapotea (2 Wafalme 2:19-25).

Tulitembelea Mlima Karmeli (Carmelite) mahali ambapo manabii walikuwa wanafundishiwa (1 Wafalme 18:19-36). Mahali hapo pia ndipo ambapo Daud alikuwa anachunga mifugo. Katika bonde lililopo hapo Karmeli, ndipo Nabii Eliya alipowaua manabii wa mungu Baali. Karmeli maana yake ni Ardhi ya Mungu. Tukiwa Karmel tuliweza kuona kwa mbali mji wa Nazareth, mahali ambapo Bikira maria alipata taarifa za kuzaliwa mtoto Yesu. Hapo pamejengwa Kanisa linaloitwa Basilica of Annunciation (announcement) lililojengwa juu ya pango waliloishi wazazi wa Bikira Maria Kwa kadri ya matukio, kuna kanisa la Annunciation, Visitation, Nativity nk). Je wajua ya kuwa Baba na mama yake Mariam waliitwa Joachim na Anna? Na kwamba Yusufu Arimathayo alimwoa dada yake Anna? Panga safari usikose.

Tuliweza kufika pia mlima Beatitudes mahali ambapo Bwana Yesu aliwapa wanafunzi wake yale mafundisho muhimu ya “Heri…….” Kama ilivyo kwenye Mathayo 5:1-12. Miongoni mwa mahubiri mazito ambayo Yesu aliwahi kutoa aliyasemea hapa, kama “waombeeni wanaowaudhi”.

Tulitembelea pia mlima Prespis mahali ambapo wayahudi walitaka kumrusha Yesu kwenye bonde la Yeziraeli kwa kuwa alikalia kiti kwenye Sinagogi ambacho hata Kuhani haruhusiwi kukaa. Alipofanikiwa kutoka eneo hilo alikimbilia Galilaya ambako pia tulifika na kuona eneo hilo ambalo karibu asilimia 75 ya muda wake katika miaka mitatu aliyofanya kazi alikuwa maeneo hayo.

Tulifika pia Kapernaum iliyo ndani ya Galilaya mahali ambapo Yesu alikuwa anakaa kwa Petro lakini pia tulifika mahali ambapo Petro aliachiwa mamlaka ya kuongoza (St Peter’s Primacy). Mahali hapa ndipo tendo lile la kugawa samaki wawili na mikate 5 lilipofanyika. Katika eneo hili tulitembelea pia Kana ya Galilaya mahali ambapo Bwana Yesu alifanya muujiza wa kwanza kwenye ile harusi. Yale mabalasi yaliyojazwa maji na kuwa divai njema. Mabalasi hayo ni halisi kabisa na bado yapo hadi leo japo yamechakaa.

Tulitembelea maeneo mengi sana ambayo si rahisi kuyaeleza yote hapa. Tumejifunza mengi sana ambayo yametuongezea uelewa katika Imani yetu ya Kikristo. Ningependa kukutia moyo Mungu akusaidie na akupe kibali uweze kufika Jerusalemu.

Mwisho wa ziara yetu tulipewa vyeti na Meya wa Yerusalemu vinavyotutambua kama “Mhujaji wa Yerusalemu” (Jerusalem Pilgrim – JP).

Bwana Atuwezeshe.

-----------------------------

PICHA NA MAELEZO: Picha na Maelezo ya Ziara

Ripoti hii imeandaliwa na JP George Israel Mnyitafu ambaye alikuwa ni mmoja wa watu walioshiriki katika ziara hiyo.