Date: 
10-12-2022
Reading: 
1Wakorintho 4:1-5

Hii ni Advent 

Jumamosi asubuhi tarehe 10.12.2022

1 Wakorintho 4:1-5

[1]Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu.

[2]Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.

[3]Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu.

[4]Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana.

[5]Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu.

Bwana anakuja katika Utukufu wake;

Mtume Paulo anawaandikia watu wa Kanisa la Korintho kuhusu huduma ya Mitume, kuwa ni huduma yenye kutunza siri za Mungu. Mtume Paulo anajiona kuwajibika mbele za Mungu kwa sababu ya huduma yake, kwa sababu Mungu ndiye ahukumuye. Paulo anawasihi watu wa Korintho kumwangalia Bwana ahukumuye kama astahiliye kuabudiwa, maana ndiye mwenye hatma ya wote waaminio.

Ujumbe wa Mtume Paulo kuhusu utumishi wa Kristo na uwakili wa siri za Mungu unatukumbusha kumwamini na kumtumikia Bwana kwa uaminifu katika maisha yetu. Yeye atakuja kwa hukumu, ndiyo maana Paulo anasema ndiye ahukumuye. Katika utume wetu tusisahau kumtumikia tukijiandaa kwa kurudi kwake, maana ajapo tena tutahukumiwa kila mmoja kwa matendo yake.

Siku njema