Date: 
10-06-2024
Reading: 
1 Timotheo 1:5-6

Jumatatu asubuhi tarehe 10.06.2024

1 Timotheo 1:5-6

5 Walakini mwisho wa agizo hilo ni upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema, na imani isiyo na unafiki.

6 Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili;

Heri wenye moyo safi;

Nyaraka za Timotheo (na Tito) huitwa "nyaraka za kichungaji" kwa sababu zimeandikwa kwa viongozi wa makanisa na kwa jumla zina malengo ya kuwashauri juu ya jinsi inavyowapasa kuziongoza Jumuiya za Kikristo. 

Waraka wa kwanza wa Timotheo una malengo mawili makuu;

Kwanza kabisa ni mwongozo kuhusu matatizo ya uongozi wa Kanisa na kupinga mafundisho ya uongo. Kwa hiyo waraka huu unatoa mawaidha kuhusu taratibu za ibada (2:1-15) sifa zinazotakiwa kutoka kwa mtu anayetaka kuwa Askofu (3:1-17) na mashemasi (3:8-13). Waraka pia unatoa mwongozo juu ya jinsi viongozi wa Kanisa wanavyopashwa kuhusika katika hali ya kujinyima anasa za mwili (4:1-10), mtazamo wao kuhusu watu mbalimbali kama wajane, wazee na watumwa (sura ya 5 na 6).

Pili; mwandishi anawaonya vikali walimu ambao wamekosa ufahamu na kupotea katika mazungumzo yasiyo na faida na mwishoni huishia katika kuizamisha imani yao (1:3-7, 19-20 na sura ya 6). Kwa namna ya pekee katika 6:3-10 Paulo anatumia maneno makali kuwaonya wale wanaojaribu kutumia dini kwa faida yao wenyewe. Yapo pia maonyo kuhusu wale waliojidai kuwa na ujuzi wa kweli na kujiona juu kuliko maumbile na hivyo kukataza kuoa na kuwataka watu waache kabisa kula vyakula fulani.

Sasa somo la asubuhi hii linaangukia katika sehemu ambayo Mtume Paulo anakazia "onyo juu ya walimu wa uongo". Paulo anamwambia Timotheo kusimamia mafundisho ya kweli. Timotheo anatakiwa kuwakataza wengine wasifundishe kinyume na Injili ya kweli.

Ndipo katika somo Paulo anasema kuwa lengo la agizo ni kuleta upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema isiyo na unafiki. Kukosa dhamira njema katika kazi ya Injili ni ubatili. Tunakumbushwa kuwa na dhamiri njema katika utume wetu, tukihubiri kweli na kutenda yote kwa Utukufu wa Mungu. Amina.

Tunakutakia wiki njema, ukiwa mwenye moyo safi.

 

Heri Buberwa Nteboya Mlutheri 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com