Date: 
08-09-2023
Reading: 
Zaburi 15:3-5

3 Asiyesingizia kwa ulimi wake. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, Wala hakumsengenya jirani yake.
4 Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana Ingawa ameapa kwa hasara yake, Hayabadili maneno yake.
5 Hakutoa fedha yake apate kula riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo Hataondoshwa milele.

Jirani wetu;

Mwandishi wa Zaburi ya 15 ni Daudi, ambapo kwa mazingira ya leo naweza kusema anajiuliza mtu aingieje ibadani? Nasema hivi kwa sababu ya mstari wa kwanza;
Zaburi 15:1. Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako? Ni nani atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu?

Mstari wa pili unasema kuwa ni yule aendaye kwa ukamilifu na kutenda haki, asemaye kweli kwa moyo wake.
Somo letu linaendelea hapo likisema kuwa ni yule asiyesingizia kwa ulimi wake, hakumtenda mwenziye mabaya wala kumsengenya jirani yake. Katika yote hayo, huyo atendaye mema hataondoshwa milele.

Zaburi inatuita kumwendea Bwana tukiwa wenye upendo kati yetu. Tuwapende jirani zetu, tuwatendee mema. Hapo ndipo tunakuwa na ibada njema mbele za Mungu. Amina.
Ijumaa njema.

Heri Buberwa 
Mlutheri