Hii ni Pentekoste
Jumamosi asubuhi tarehe 03.06.2023
1 Wakorintho 14:26-33
26 Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga.
27 Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri.
28 Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu.
29 Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue.
30 Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze.
31 Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe.
32 Na roho za manabii huwatii manabii.
33 Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.
Roho Mtakatifu msaada wetu;
Mtume Paulo anawaandikia Wakorintho kuhusu utaratibu wakati wa kusanyiko, au ibada. Anawausia kufanya ibada kwa nia ya kujenga, yaani kumwabudu Mungu kwa pamoja. Kunena kwa lugha kuwe kwa zamu kwenye utararibu na tafsiri, maana ibada lazima ifanyike baraka kwa wote. Mtume Paulo anakazia kuwa kufunuliwa kwa mmoja kusivuruge ibada, bali kuwepo umoja na kusikilizana ili ibada iwe baraka kwa wote.
Ujumbe huu unatukumbusha kumwabudu Bwana kwa pamoja katika Roho na kweli, kwa utaratibu pasipo kelele na fujo. Ibada ifanyike kwa lengo la kumwabudu Mungu pekee, kwa ushirika wa pamoja katika kuzingatia taratibu za pamoja. Hakuna sehemu isiyokuwa na utaratibu, hata Mungu ni wa utaratibu, hivyo na ibada ifuate taratibu. Tumwabudu Mungu peke yake, kwa Utukufu wake, katika ushirika wetu.
Jumamosi njema.
Heri Buberwa