Date: 
19-12-2022
Reading: 
Luka 1:22-28

Hii ni Advent 

Jumatatu asubuhi tarehe 19.12.2022

Luka 1:26-38

26 Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti,

27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.

28 Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.

29 Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?

30 Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.

31 Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.

32 Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.

33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.

34 Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?

35 Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.

36 Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa;

37 kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.

38 Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

Bwana yu karibu;

Malaika Gabriel alimletea habari Mariamu kuwa angebeba mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kuzaa mtoto ambaye angemwita Yesu. Huyo ndiye angekuja kuwaokoa watu na dhambi zao. Hii ilikuwa ni kuelekea ukamilifu wa mpango wa Mungu katika kumwokoa mwanadamu, kwa kumtuma Yesu Kristo.

Baadaye Yesu alizaliwa Bethlehemu kwenye hori la ng'ombe wakati wa sensa iliyofanyika kwa amri ya Kaisari. Baada ya kuja, alifanya kazi ya kufundisha, kuhubiri na kuponya akijenga ufalme wa Mungu. Alipomaliza kazi yake alipaa mbinguni. Lakini hadi leo, Yesu yupo maana hukaa kwetu. Hata leo anabisha kuingia mioyoni mwetu, ili akae kwetu.

Yesu huyu ndiye atarudi tena kulichukua Kanisa. Anapobisha kuingia kwetu anataka tuwe tayari ili akirudi asituache. Hivyo andaa moyo wako, tayari kuingia kwenye ufalme wa Mungu maana Bwana yu karibu.

Uwe na wiki njema.