Date: 
12-05-2023
Reading: 
2 Mambo ya nyakati 29:28-30

Hii ni Pasaka 

Ijumaa asubuhi tarehe 12.05.2023

2 Mambo ya Nyakati 29:28-30

28 Na kusanyiko lote wakaabudu, waimbaji wakaimba, wenye mapanda wakapiga; haya yote yakaendelea hata ilipomalizika sadaka ya kuteketezwa.

29 Hata walipokwisha kutoa sadaka, mfalme, na hao wote waliokuwapo naye, wakasujudia, wakaabudu.

30 Tena Hezekia mfalme na wakuu wakawaamuru Walawi, wamwimbie Bwana sifa kwa maneno ya Daudi, na ya Asafu mwonaji. Wakaimba sifa kwa furaha, wakainama vichwa, wakaabudu.

Kila aliye hai amsifu Bwana;

Hezekia alianza kutawala akiwa na miaka ishirini na tano, akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana. Aliwaita watu kumtolea Bwana sadaka ya kuteketezwa. Ndipo tunaona katika somo sadaka ikitolewa na wimbo wa sifa kwa Bwana ukiimbwa. Hezekia aliwaongoza watu kumcha Bwana, ndiyo maana aliwaita kumtolea sadaka na kumwimbia sifa.

Yesu Kristo alipotukomboa kwa njia ya kifo msalabani alitufanya tuokoke. Lakini hakuishia hapo, hukaa nasi hata leo. Kwa nini tusiishi tukimpendeza yeye? Kwa nini tusimtolee sadaka? Kwa nini tusimwimbie wimbo wa sifa? Tuishi kwa kumwabudu na kumshukuru Mungu maana alituokoa na hutulinda kuelekea uzima wa milele.

Siku njema.

 

Heri Buberwa