Date: 
10-05-2023
Reading: 
Ufunuo wa Yohana 15:1-4

Hii ni Pasaka 

Jumatano asubuhi tarehe 10.05.2023

Ufunuo wa Yohana 15:1-4

1 Kisha nikaona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia.

2 Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu.

3 Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa.

4 Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.

Kila aliye hai amsifu Bwana;

Asubuhi ya leo tunasoma Yohana akifunuliwa kuona walioshinda wakiimba wimbo wa Musa, wimbo wa Mwana-Kondoo. Wanamsifu Mungu wakisema matendo yake ni ya ajabu na haki zake ni za kweli. Wanalitukuza jina la Bwana na kumuita Mtakatifu mwenye nguvu.

Yohana alifunuliwa kuona walioshinda wakimsifu Bwana. Tukiishi maisha ya ushindi tutamuona Bwana na tutaimba wimbo wa sifa mbele ya kiti cha enzi. Maisha yenye ushuhuda ndiyo njia ya kuuona ufalme wa Mungu, ambapo tutaimba wimbo wa sifa milele yote. Siku njema.

 

Heri Buberwa 

Mlutheri