Date: 
08-05-2023
Reading: 
Zaburi 98:1-4

Hii ni Pasaka 

Jumatatu asubuhi tarehe 08.05.2023

Zaburi 98:1-4

1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.

2 Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.

3 Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.

4 Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.

Kila aliye hai amsifu Bwana;

Zaburi tunayoisoma leo ni wimbo ulioimbwa na Israeli wakimshangilia Bwana baada ya kutoka uhamishoni. Waliona kuwa Bwana ndiye aliyewawezesha kutoka uhamishoni. Waliziona rehema za Bwana na uaminifu wake hadi kuwaokoa. Waliimba, walimsifu Bwana, lakini waliendelea kuwaita wengine kumsifu Bwana.

Zaburi hii huwa tunaiimba wakati wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Huwa tunashangilia kuzaliwa kwa Yesu, kama Mwokozi aliyekuja kutuokoa na dhambi zetu. Kumbe pale huwa tunakumbushwa kuwa Yesu alizaliwa kwa ajili yetu ili tuokolewe kutoka dhambini. Kwa njia hii yeye ni Mwokozi wetu astahiliye sifa, ndiyo maana tunaelekezwa kumpa sifa zetu. Sifa iliyo kubwa zaidi ni kuishi maisha yampendezayo.

Uwe na wiki njema yenye ushuhuda 

 

Heri Buberwa