Date: 
04-05-2023
Reading: 
1 Wathesalonike 2:13-16

Hii ni Pasaka 

Alhamisi asubuhi tarehe 04.05.2023

1 Wathesalonike 2:13-16

13 Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.

14 Maana ninyi, ndugu, mlikuwa wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyo katika Uyahudi, katika Kristo Yesu; kwa kuwa mlipata mateso yale yale kwa watu wa taifa lenu wenyewe, waliyoyapata na hao kwa Wayahudi;

15 ambao walimwua Bwana Yesu, na hao manabii, na kutuudhi sisi; wala hawampendezi Mungu, wala hawapatani na watu wo wote;

16 huku wakituzuia tusiseme na Mataifa wapate kuokolewa; ili watimize dhambi zao siku zote. Lakini hasira imewafikia hata mwisho.

Maisha mapya ndani ya Yesu;

Ni sala ya Mtume Paulo akimshukuru Mungu kwa kuwa alipotumwa kwenda Thesalonike alienda kuhubiri neno la Mungu, nao watu wa Kanisa la Thesalonike walilipokea neno hilo kama neno la Mungu. Anawapongeza kuacha imani ya Kiyahudi na kumfuata Yesu Kristo kwa njia ya neno lake. Anawataka kutoacha kumshuhudia Kristo.

Asubuhi hii tukumbuke kuwa Injili inayohubiriwa kwetu Kanisani ndiyo neno la Mungu, ndiyo Injili ya kweli. Basi na tuipokee Injili hiyo kama neno la Mungu, na neno hilo likae kwa wingi mioyoni mwetu ili tuwe na maisha mapya siku zote. Amina.

Siku njema.

 

Heri Buberwa 

Mlutheri