Wanawake AZF waongoza Ibada ya Kwaresma

Wanawake usharikani walishiriki katika kuongoza ibada ya Kwaresma iliyofanyika siku ya Jumatano tarehe 9/3/2022, ibada hiyo ilifanyika kwa kutumia kitabu maalum cha maombi ya dunia cha mwaka huu, ambapo ibada kuu ya maombi hayo ilifanyika siku ya Ijumaa tarehe 4/3/2022 ambayo yalishirikisha wanawake wote duniani.

Ibada hii ya usharikani iliongozwa na Mama Veronica Kileo na mahubiri yalitolewa na Bibi Jacqueline Swai, neno kuu katika ibada hii ya maombi lilitoka katika kitabu cha nabii Yeremia 29:11.

Wanawake AZF washiriki Maombi ya Dunia

Kila mwaka wanawake wote wa kikristo duniani, huungana na kufanya maombi kwa pamoja kwa kuombea amani duniani, ushirikiano, upendo, kuombea familia na kazi za kanisa, maombi haya huandaliwa na nchi iliyoteuliwa kwa kupata zamu ya kuandaa.

Mwaka huu  maombi hayo yaliandaliwa na wanawake wa nchi ya Uingereza, katika mkoa wa Dar es Salaam, maombi hayo yalifanyika siku ya Ijumaa tarehe 4/3/2022 katika viwanja Saba Saba ambayo yalisimamiwa na dhahebu la Baptist, Wanawake wengi walishiriki maombi hayo wakitokea katika madhehebu mbalimbali ya kikristo likiwemo dhehebu la Kilutheri.

Mradi wa Ufugaji Nyuki: Mambo YAMEIVA!

Hivi karibuni, viongozi wa Umoja wa wanawake wakishirikiana na wanawake wote usharikani, walizindua mazao yatokanayo na mradi wa ufugaji wa nyuki.

Mradi huo ambao una jumla ya mizinga ipatayo arobaini, upo katika mtaa wa Tabora ambao unatunzwa na usharika wa Azania Front Cathedral,mradi huo umeweza kuwapatia mazao mengi yakiwemo asali, masega, juice na nta iliyoweza kutengeneza mishumaa. Mradi huo ni mradi endelevu ambao asali na mazao yake huvunwa kila baada ya miezi mitatu.