Date: 
19-07-2022
Reading: 
Yoshua 1:12-18

Jumanne asubuhi tarehe 19.07.2022

Yoshua 1:12-18

[12]Tena Yoshua akawaambia Wareubeni, na Wagadi, na hao wa nusu ya kabila ya Manase, akasema,

[13]Likumbukeni neno lile alilowaamuru Musa mtumishi wa BWANA, akisema, BWANA, Mungu wenu, anawapa ninyi raha, naye atawapa nchi hii.

[14]Wake zenu, na watoto wenu, na makundi yenu, watakaa katika nchi aliyowapa Musa ng’ambo ya Yordani; bali ninyi mtavuka mbele ya ndugu zenu, hali mmevikwa silaha zenu, watu wote wenye nguvu, na ushujaa, ili mpate kuwasaidia;

[15]hata BWANA atakapowapa ndugu zenu raha, kama alivyowapa ninyi, na wao pia wamepata kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wenu; ndipo mtakapoirudia nchi ya milki yenu na kuimiliki, ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwapeni ng’ambo ya Yordani upande wa maawio ya jua.

[16]Wakamjibu Yoshua, wakasema, Hayo yote uliyotuamuru tutayafanya, na kila mahali utakakotutuma tutakwenda.

[17]Kama vile tulivyomsikiliza Musa katika mambo yote, ndivyo tutakavyokusikiliza wewe; BWANA, Mungu wako, na awe pamoja nawe tu, kama alivyokuwa pamoja na Musa.

[18]Kila mtu atakayeiasi amri yako, asiyasikilize maneno yako katika mambo yote utakayomwamuru, atauawa. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, hilo tu.

Tunaitwa kuwa wanafunzi na wafuasi;

Ni maandalizi ya kuvuka mto Yordani, ambapo Yoshua anatoa maelekezo jinsi ambavyo Israeli wangevuka. Israeli walikubali na kupokea maelekezo ya Yoshua wakisema kufanya walivyoamriwa, na kwenda kokote ambapo wangetumwa. Walikiri kumsikiliza Yoshua kama ambavyo walimsikiliza Musa. Walizidi kumtia moyo kiongozi wao Yoshua wakimwambia "uwe hodari na moyo wa ushujaa, hilo tu".

Somo hili linatukumbusha utii kwa neno la Mungu katika ufuasi wetu. Uanafunzi mzuri ni kusoma, kusikiliza na kujifunza neno la Mungu, ndipo tunakuwa na nguvu ya kusimama kama wafuasi wazuri. 

Ni wito wangu kwako asubuhi hii kuwa mtii wa neno la Mungu, ili uwe mfuasi kamili wa Yesu Kristo.

Siku njema