Jumatano asubuhi tarehe 08.02.2023
Waefeso 2:11-17
11 Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono;
12 kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani.
13 Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.
14 Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga.
15 Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani.
16 Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba.
17 Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu.
Tunaokolewa kwa neema;
Mtume Paulo anawakumbusha watu wa Efeso jinsi walivyomuona asiyetahiriwa kuwa wa mataifa. Anawaambia kuwa tohara iliwatenga mbali na Bwana, lakini kwa damu yake Yesu Kristo kila mmoja ameokolewa. Paulo anakazia kuwa msingi wa wokovu kwa wanadamu ni damu ya Yesu, na siyo maagano mengine yoyote.
Ujio wa Yesu Kristo uliwaunganisha waliokuwa mbali na wale waliokuwa karibu. Yesu aliondoa mipaka kwa wanadamu, maana kwa damu yake wote waliokolewa. Mkazo wa Paulo asubuhi hii ni kuwa kwa neema ya Mungu sote tumestahili wokovu ambapo sheria na maagano havina nafasi tena. Mwamini Yesu uokolewe, maana tunaokolewa kwa neema.
Siku njema.
Heri Buberwa