Alhamisi asubuhi tarehe 27.11.2025
Malaki 3:1-5
1 Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi.
2 Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo;
3 naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki.
4 Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
5 Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema Bwana wa majeshi.
Uzima wa milele upo kwa ajili yako;
Somo la leo ni utabiri wa Malaki juu ya ujio wa Yohana Mbatizaji ambaye alikuja kuleta habari za ujio wa Yesu Kristo, ujumbe ambao uliwataka watu kujiandaa kumpokea Mesiya ajaye, Yesu Kristo. Utabiri huu upo katika unabii wa Isaya, lakini pia unanukuliwa na Marko Mtakatifu;
Marko 1:2
Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako.Malaki anamtabiri Yesu atakayekuja kuukomboa ulimwengu, akirudi kwa hukumu ya watu wake. Anaonesha kwamba ipo hukumu akiuliza kwamba ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Malaki anaonesha ukuu wa Yesu Kristo Mwokozi, ambaye tukimwamini tutaurithi uzima wa milele. Amina
Alhamisi njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
