Date: 
06-08-2024
Reading: 
Malaki 2:4-7

Jumanne asubuhi tarehe 06.08.2024

Malaki 2:4-7

4 Nanyi mtajua ya kuwa mimi nimewapelekeeni amri hii, ili agano langu liwe na Lawi, asema Bwana wa majeshi.

5 Agano langu naye lilikuwa agano la uhai na amani; nami nikampa ili aogope, naye akaniogopa, akalicha jina langu.

6 Sheria ya kweli ilikuwa kinywani mwake, wala udhalimu haukuonekana midomoni mwake; alikwenda pamoja nami katika amani na unyofu, na kuwageuza wengi hata wakaacha uovu.

7 Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa, tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake; kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Bwana wa majeshi.

Enendeni kwa hekima;

Malaki anawaonya makuhani kwa mienendo yao isiyofaa katika huduma yao. Wakati Malaki anaandika ujumbe huu, makuhani hawakuzingatia kulitukuza jina la Bwana, wakati wao ndiyo walitakiwa kuwaongoza watu kumwelekea Bwana! Malaki aliwaambia kuwa kwa mienendo yao isiyofaa wangeondolewa kwenye nafasi yao ya ukuhani! (2)

Somo linaonesha kuwakumbusha makuhani kuzingatia Agano la kumcha Bwana. Makuhani wanatakiwa kuhifadhi maarifa na kuishika sheria, ili wawaongoze watu kumcha Bwana. Naweza kusema kuwa kwa kutomcha Bwana, makuhani hawakuwa na hekima. Hekima itokayo kwa Mungu huwaongoza waaminio kumwanini na kumcha Bwana. Tumuombe Mungu atupe hekima yake ituingizayo katika uzima wa milele. Amina

Jumanne njema.

Heri Buberwa