Jumamosi asubuhi tarehe 15.06.2024
Yakobo 1:19-27
19 Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika;
20 kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.
21 Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
22 Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.
23 Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.
24 Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.
25 Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.
26 Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai.
27 Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.
Heri wenye moyo safi;
Yakobo anafundisha kuwa mtu asiwe mwepesi wa kusema wala kukasirika, bali awe mwepesi wa kusikia. Yakobo anatoa sababu, kwamba hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu. Na mimi naongezea, kwamba kwa sababu imani huja kwa kusikia, kusikiliza zaidi kunatupa nafasi zaidi ya kusikia tafakari ya neno la Mungu, hivyo kukuza imani yetu. Msisitizo wa Yakobo ni kwa watu kuwa watendaji wa neno, na siyo kuwa wasikiaji tu, maana hiyo ni kujidanganya nafsi zao.
Ujumbe wa Yakobo asubuhi hii ni kuwa makini katika kusikiliza ili kufanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi. Lakini pia kuwajibika, yaani kutimiza wajibu wetu katika maisha ya imani. Kristo atuwezeshe kusikia na kuamua kwa usahihi ili tuwe na moyo safi, tayari kuurithi uzima wa milele. Amina
Siku njema
Heri Buberwa