Date: 
23-05-2023
Reading: 
Kumbukumbu la Torati 9:25-29

Jumanne asubuhi tarehe 23.05.2023

Kumbukumbu la Torati 9:25-29

25 Ndipo nikaanguka nchi mbele za Bwana siku zile arobaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka nchi; kwa kuwa Bwana alisema atawaangamiza.

26 Nikamwomba Bwana, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu.

27 Wakumbuke watumwa wako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie upotofu wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao;

28 isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu Bwana hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowapa ahadi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, alivyowatoa nje ili kuwaua jangwani.

29 Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka.

Usikie kuomba kwetu;

Kazi ya kuwaongoza wana wa Israeli kuelekea nchi ya ahadi haikuwa rahisi kwa Musa. Walimsumbua sana maana ilifikia hatua Bwana akasema yafuatayo;

Kumbukumbu la Torati 9:13-14

13 Tena Bwana akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu;
14 niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao.

Sasa baada ya ujumbe huo wa Bwana ndipo tunasoma Musa akianguka mbele za Bwana, anaomba Bwana asiwaangamize Israeli. Anamuomba Bwana awakumbuke, asiangalie dhambi zao maana ni watu wake. Yaani Musa anawaombea msamaha kwa Mungu. Ukiendelea kusoma unaona Bwana akiwasamehe na kumpa Musa amri zake ili awape watu wake.

Musa alipoona Israeli wamemkosea Mungu aliwaombea msamaha kwa Mungu. Lipo fundisho la kumwendea Bwana kwa imani tukiomba msamaha wa dhambi pale tunapomkosea. Tunapotubu dhambi zetu Yesu hutupokea na kutusamehe, maana yeye ameahidi kusikia kuomba kwetu. Dumu katika sala ukifanya toba ya kweli. Amina

Siku njema.

 

Heri Buberwa