Hii ni Kwaresma
Jumamosi asubuhi tarehe 25.03.2023
Marko 8:1-9
1 Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia,
2 Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula;
3 nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali.
4 Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani?
5 Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba,
6 Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; wakawaandikia mkutano.
7 Walikuwa na visamaki vichache; akavibarikia, akasema wawaandikie na hivyo pia.
8 Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba.
9 Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga.
Yesu ni chakula cha uzima;
Katika uandishi wake, Marko alipendelea ishara alizozifanya Yesu. Ameandika jumla ya ishara 18, 13 katika sura 7 za kwanza, ishara ya 14 ni katika sura ya 8 (somo la leo). Kulisha watu elfu nne kunaendana na ishara ya kulisha watu elfu tano (sura ya 6). Baadhi ya wahubiri hudhani ni tukio lile lile, kwamba labda mwandishi alichanganya,au ameandika mara mbili kuelezea tukio moja. Hiyo haiwezekani! Biblia haina makosa, na haielezei vitu kutokea, ambavyo havikutokea kuleta habari tu!
Kulisha watu elfu nne na kulisha wale elfu tano, pamoja na kufanana, ni matukio mawili tofauti. Jaribu kusoma na kulinganisha kwa umakini. Kama haitoshi, Yesu mwenyewe anayarejea kama matukio mawili tofauti;
Marko 8:19-20
[19]Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili. [20]Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba.Tukio hili sio la kushangaza. Nyakati zote katika Biblia, Mungu hakuwahi kuwatupa watu wake.
Mfano; Kumbuka katika Agano la kale Mungu alipowatoa wana wa Israeli Misri, jangwani bila chakula. Mungu alishusha mana kila siku. Mungu alifanya ishara hii kila siku. (Kutoka 16)
Miaka 600 kabla katika tukio kama hili la kulisha watu elfu nne, kuna mtumishi alipeleka mikate 20 kwa Elisha, Elisha akaamuru mikate watu Mia waliokuwa mbele yake wale. Wakala na kusaza.
2 Wafalme 4:42-44
[42]Tena, akaja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale. [43]Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa BWANA asema hivi, Watakula na kusaza. [44]Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la BWANA.Yesu hakufanya ishara mpya kuwalisha watu elfu nne, na hakuwa amepanga kufanya hivyo. Alichofanya ni kuwahudumia watu aliokuwa nao, akiunganisha tukio hili na maandiko matakatifu, kuwa Mungu anawajali watu wake.
Katika somo hili tunaona yafuatayo;
1. Huruma ya Yesu (mst 1-3)
Yesu anadhihirisha kuwa yeye ni mwenye huruma. Watu aliokuwa nao kwa siku tatu anaona bora kwanza wale ndio waondoke. Mpaka inafikia hatua hii, inawezekana;
-Labda kuna waliomfuata kumuomba chakula
-Labda eneo lenyewe lilikuwa halina chakula, maana ilikuwa nyika
-Labda kuna waliomlilia njaa
- Labda aliona wamechoka na hawawezi kurudi nyumba ni kwao n.k
Vyovyote vile, hapa tunajifunza kuwa Yesu ni mwenye huruma. Tunapoendelea na tafakari ya majira haya, tunakumbushwa kumwendea Yesu mwenye huruma, lakini nasi pia kuwa na huruma kwa wenzetu. Huruma ianzie kwetu. Haiwezekani tukose huruma, halafu tuombe huruma. Tuishi kwa kuhurumiana, ndipo Taifa la Mungu litastawi.
2. Utoaji wa Yesu (mst. 4-7)
Yesu alijua watu wana njaa, na alijua ana uwezo wa kuwapa chakula, akawapa.
Yaani alitoa alichokuwa nacho.
Kwa kifupi tu, wewe unatoa ulicho nacho kuwasaidia wengine?
3. Yesu anatosha. (mst 8-9)
Yesu anatoa chakula na walaji wanasaza. Wanafunzi waliogopa hata watu wasubiri kula, lakini Yesu anawapa chakula na wanasaza. Wanafunzi walitumia akili zao kuwa chakula hakipo! Kumbe hawakujua kuwa hawakujitosheleza, ila Yesu angetosha.
Wanafunzi walichotakiwa kujua ni kuwa katika huduma yao walitakiwa kumtegemea Yesu ili kuutimiza utume wao. Kitendo cha wanafunzi kuuliza watu watakula nini, ni dhahiri waliamini hawawezi kuwahudumia wale watu. Hawakukumbuka kuwa Yesu hashindwi lolote.
Katika maisha yetu, tunahitaji Yesu atuongoze ili tuweze kuifanya kazi yake. Haiwezekani kazi ya Mungu tukaifanya kwa nguvu zetu wenyewe. Bila Yesu hatujitoshelezi!
Ndio maana tunaambiwa kuwa Yesu ni chakula cha uzima.
Ndugu yangu;
Yesu ndiye chakula kilichoshuka kutoka juu kwa ajili ya wanadamu wote. Mwamini Yesu aliye chakula cha uzima, ili uupate huo uzima.
Jumamosi njema
Heri Buberwa