Alhamisi asubuhi tarehe 19.01.2023
Yohana 19:25-30
[25]Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene.
[26]Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao.
[27]Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.
[28]Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu.
[29]Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.
[30]Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.
Nyumba zetu hubarikiwa na Mungu;
Bwana Asifiwe;
Somo la leo asubuhi linahusisha baadhi ya maneno ya Yesu msalabani kama ifuatavyo;
Mstari wa 26 na 27 ni neno la 3, Yesu akimwambia mama yake; mtazame mwanao. Pia akimwambia mwanafunzi yule aliyempenda; tazama mama yako.
Hili ni neno la mahusiano mema (Relationship). Yesu alimuona mwanafunzi aliyempenda akiwa amesimama na mama yake, anawaambia kila mmoja kumtazama mwingine. Yesu anatufundisha kupendana tukiishi pamoja kama familia moja ya Kristo. Sisi ni Taifa la Mungu
Mstari wa 28 na 29, Yesu anasema; Naona kiu;
Hili ni neno la dhiki (distress). Yesu anajisikia na kujiona mwenye dhiki. Kama mwanadamu, damu ilimtoka nyingi hivyo alihisi kiu, akapewa siki. Kama Mungu, Yesu alikuwa na kiu ya upendo wa Baba yake aliyemuacha aimalize kazi aliyomtuma aifanye. Anaona kiu ya upendo na wokovu kwa watu wake.
Yesu alikuwa anafanya alichokihubiri. Sisi tunafanya tunayoyahubiri? Tunapendana katika familia zetu?
Mstari wa 30 Yesu anasema Imekwisha;
Hili lilikuwa neno la ushindi (Triumph). Ni tangazo la mwisho wa maisha ya Yesu duniani kabla ya ufufuo. Yesu alikuwa kamaliza kazi iliyomleta. Njia ya wokovu ilikuwa imekamilika, iliyojaa upendo timilifu kwa wote.
Maneno haya ya Yesu yote yaliashiria upendo wake kwetu alipokuwa akikiendea kifo msalabani kwa ajili yetu. Nasi tunaalikwa kuuiga mfano huu wa upendo wa Yesu kwenye familia zetu ili baraka zake ziambatane nasi.
Siku njema.