Wazee wa Baraza wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral tarehe 9 Julai 2022 walifanya ziara katika mtaa wa Tabora ili kujionea maendeleo ya mtaa huo na mradi wa ujenzi wa nyumba ya ibada unavyoendelea mtaani hapo. Wakiwa katika mtaa huo Wazee wa Baraza walipata maelezo mafupi juu ya maendeleo ya ujenzi wa nyumba ya ibada
kutoka kwa mhandisi wa mradi huo. Katika maelezo yake mhandisi huyo alisema mradi utakamilika mnamo mwezi Oktoba mwaka huu iwapo hakutakuwa na changamoto za upatikanaji wa vifaa na fedha kwa ajili ya kukamilisha sehemuiliyobakia.
Wazee wa Baraza walipata fursa ya kutembelea na kukagua mradi huo ambapo, kwa pamoja walikubaliana kuchangia fedha takribani milioni 20 kwa ajili ya kumalizia sehemu iliyobaki ili jengo liweze kukamilika na kuwa tayari kwa matumizi.
Akizungumza mtaani hapo, Mchungaji Kiongozi wa Usharika Mchungaji Charles Mzinga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la usharika aliwashukuru wajumbe wote kwa kutenga muda wao na kufika katika eneo hilo la mradi ili kujioneaa kazi inavyoendelea. Pia aliwashukuru kwa kuendelea kutoa michango mbalimbali ili kuwezesha kukamilika kwa mradi huo.
“Nawashukuru wajumbe wote kwa kuweza kufika hapa Tabora na kujionea maendeleo ya mradi huu, sasa ni dhahiri kwamba tumepiga hatua kubwa, ni matarajio yangu kwamba kama kila kitu kitakwenda kama tulivyopanga basi tutarudi wote mahali hapa mwezi Oktoba mwaka huu kwa ajili ya kuzindua jengo hili ili liweze kuwahudumia ndugu zetu wa mtaa wa Tabora na maeneo ya jirani,” alisema Mchungaji Charles Mzinga.
------------------------------------------
Matukio katika picha wakati wa ziara ya Wazee wa Baraza walipotembelea mtaa wa Tabora kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya ibada.