Event Date: 
12-08-2022

Siku ya Jumapili tarehe 10 Julai 2022 ilikuwa ni Siku ya Vijana katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka ili kutambua na kuthamini mchango wa vijana katika kulijenga na kuliendeleza neno la Bwana.

Katika siku hiyo muhimu kwa vijana na usharika kwa ujumla, vijana wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front walipata fursa ya kuongoza ibada zote tatu za siku hiyo zilizoambatana na igizo kutoka kwa vijana hao.

Kwa ibada za Kiswahili, Anna Kayumbo aliongoza Litrugia na Dickson Mwakisu aliongoza mahubiri huku Israel Mwinyitafu akisoma matangazo ya Usharika.

Akitoa neno la siku hiyo, Ndugu Dickson Mwakisu aliwaasa vijana wenzake kuwa makini na teknolojia ya kisasa na kwamba wamtegemee Mungu katika kila wanalolifanya. ”Hata kama teknolojia ya kisasa inatusaidia kupata pesa lakini inabidi tuwe makini na jinsi tunavyoitumia.”

Ndugu Dickson pia aliwaasa vijana wenzake kuwa na nidhamu ya matumizi ya pesa na kwamba wasiishi kwa kuiga maisha ya watu wengine au kutaka kuonekana wana maisha mazuri hasa wanapokuwa wakitumia mitandao ya kijamii.

Mchungaji kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral Mchungaji Charles Mzinga aliwapongeza vijana kwa kuendelea kushirikiana na washarika wengine katika kazi ya Mungu na namna wanavyojitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za za usharika na kanisa kwa ujumla.

------------------------------

PICHA. Ibada ya Vijana AZF