Date: 
18-11-2025
Reading: 
2 Petro 2:1-8

Jumanne asubuhi tarehe 18.11.2025

2 Petro 2:1-8

1 Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.

2 Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa.

3 Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.

4 Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu;

5 wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu;

6 tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya;

7 akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu;

8 maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria;

Jiandae kwa hukumu ya mwisho;

Petro anaonya juu ya manabii wa uongo waliokuwapo tangu kale, ambao anasema watakuwepo ili kuwapoteza watu wa Mungu. Anaonya kwamba wakristo wasiwaamini. Petro anasema kama Mungu hakuwaachia watu wake wapotee akawapa njia sahihi, ni muhimu kwa waaminio kumtazama Bwana kwa ajili ya uzima wa milele. Petro anakumbusha kuangamizwa kwa Sodoma na Gomora kwa sababu ya watu ambao hawakumcha Mungu.

Petro anarejea ukweli mtupu, manabii na walimu wa uongo wamejaa kila mahali leo. Hawahubiri wokovu kwa neema ya Mungu, bali kukombolewa kwa sadaka. Wanahubiri sadaka kwa ajili ya matumbo yao. Hawana muda na kondoo. Hawa wakipewa nafasi watu watakosa neno la Mungu waangamie. Kwa kutoamini na kumkosea Mungu, Sodoma na Gomora palichomwa moto. Kwa kutoamini na kumkosea Mungu tutaukosa uzima wa milele. Basi tusiiache imani yetu, tukijiandaa kwa hukumu ya mwisho. Amina

Jumanne njema

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com