Ijumaa asubuhi tarehe 24.10.2025
Matendo ya Mitume 5:22-33
22 Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari,
23 wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani.
24 Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo.
25 Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu.
26 Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe.
27 Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza,
28 akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.
29 Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.
30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti.
31 Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi.
32 Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.
33 Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua.
Imani Iletayo ushindi;
Mitume walikuwa wametupwa gerezani kwa sababu ya kuhubiri Injili ya Yesu Kristo. Wakiwa gerezani malaika wa Bwana akaja akawatoa usiku, akawatuma kuendelea kuhubiri hekaluni. Wakaendelea kuhubiri na kufundisha hekaluni.
Somo linaanzia hapa, kwamba watumishi wanaenda kuwatoa mitume gerezani na wanawakuta hawapo. Walinzi walikutwa wakilinda gereza, lakini mitume wakiwa hawapo gerezani! Majemedari na makuhani wakawa na wasiwasi juu ya jambo hili. Ndipo wakapata taarifa kwamba mitume wako wanafundisha hekaluni
Jemedari mmoja alienda akawaleta kutoka hekaluni na kuwaleta barazani. Kuhani Mkuu akawauliza kwa nini waliendelea kufundisha kwa jina la Yesu? Jibu la Petro na mitume wenzake lilikuwa la kuvutia, kwamba "Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu". Jibu hili lisingetoka kwa watu wasio na imani. Inatufundisha kutoikana imani katika hali yoyote. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
