Jumatano asubuhi tarehe 30.07.2025
1 Wakorintho 13:1-13
1 Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.
2 Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.
3 Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.
4 Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;
5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;
6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;
7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.
8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.
9 Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu;
10 lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika.
11 Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.
12 Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.
13 Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.
Mambo yote yatendeke katika upendo wa Kristo;
Somo la siku ya leo asubuhi ni andiko la Mtume Paulo kwa watu wa Korintho kuhusu karama ya upendo. Aliiona jamii ya Kanisa la Korintho ilivyoishi, mwanzoni kabisa akawaandikia kuhusu migawanyiko iliyokuwa kati yao (sura ya kwanza). Watu walijigawa katika makundi. Baadaye akaja kuwaandikia juu ya upendo. Katika somo tunaona akiwaambia kuwa imani, unabii, utajiri, kunena kwa lugha n.k vyote vikifanyika bila upendo ni kazi bure.
Paulo anaendelea kuonesha matokeo ya upendo kama vile uvumilivu, adabu, fadhili, kuondoa majivuno, kutohesabu mabaya n.k Paulo anamalizia kwa kuwasihi watu wa Korintho kudumu katika imani, tumaini, upendo, lililo kuu likiwa upendo. Nasi tukumbuke amri kuu ambayo ni upendo. Amina
Jumatano asubuhi
Heri Buberwa
Mlutheri