Date: 
25-07-2025
Reading: 
1 Yohana 5:18-21

Ijumaa asubuhi tarehe 25.07.2025

1 Yohana 5:18-21

18 Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi.

19 Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.

20 Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.

21 Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.

Tudumu katika fundisho la Kristo;

Somo la asubuhi hii ni hitimisho la waraka wa kwanza wa Yohana akisema kwamba kila aliyezaliwa na Mungu hujilinda na dhambi. Yohana anaendelea kuandika kwamba wote waaminio ni wa Mungu na wasioamini hukaa katika mwovu. Yohana anasema kuwa Mungu amewapa watu wake akili ili wamjue yeye kama Mungu wa kweli, maana ndiye atakayewapa uzima wa milele.

Asubuhi hii tunakumbushwa kujilinda na dhambi. Kujilinda na dhambi bila msaada wa Mungu ni kujidanganya. Kumbe tunatakiwa kila wakati kumtegemea Mungu ili atuwezeshe kushinda dhambi. Tusipoomba msaada wa Mungu kushinda dhambi tutakaa katika mwovu kama Yohana anavyosema. Ni kwa njia ya fundisho la Kristo tunashinda na kuurithi uzima wa milele. Amina. 

Ijumaa njema

 

Heri Buberwa