Date: 
23-07-2025
Reading: 
Mathayo 5:17-19!

Jumatano asubuhi tarehe 23.07.2025

Mathayo 5:17-19

17 Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.

18 Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie.

19 Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.

Tudumu katika fundisho la Kristo;

Baadhi ya makanisa na wahubiri huchukua mistari ya somo tulilosoma kama msingi wa torati, kwamba Yesu hakuitangua torati hivyo ichukuliwe kama ilivyo. Wanasema mstari wa 17 uko wazi na ule wa 19 unakazia kutovunja amri. Lakini hawasemi kwamba kama ni torati Yesu ndiye utimilifu wa torati, na kama ni sabato Yesu ndiye bwana wa sabato.

Yesu aliongea vile, lakini akaendelea kuitimiliza torati. Ukiendelea unaona akifundisha juu ya mambo kadhaa mfano;

‐Uzinzi-hapo kale walisema usizini, lakini Yesu anasema ukitazama kwa macho ukatamani tayari umezini (5:27-30)

‐Hasira iliruhusiwa, Yesu anafundisha kusamehe (5:21-26)

‐Talaka iliruhusiwa, Yesu anazuia (5:31-32)

‐Zamani kisasi kiliruhusiwa, Yesu anafundisha kutolipiza kisasi (5:38-42) 

-Zamani adui alichukiwa, Yesu anafundisha upendo kwa adui (5:43-48)

Nimeandika mifano halisi michache, ukisoma hotuba nzima ya mlimani (sura 5 hadi 7) unaona Yesu anavyoitimiliza torati. Na baada ya kufundisha akiwaambia wamwamini yeye. Angalia alivyosema mwishoni kwenye hotuba ya mlimani;

Mathayo 7:24-27

24 Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;
25 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.
26 Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;
27 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.

Kwa hiyo Yesu baada ya kuelekeza jinsi ya kuenenda katika ufalme wa Mungu, anajitambulisha kama mwokozi wa ulimwengu. Wito wa asubuhi hii ni kumwamini Yesu Kristo aliye utimilifu wa torati. Kwa kudumu katika fundisho lake ametuahidi uzima wa milele. Amina

Jumatano asubuhi 

Heri Buberwa