Ijumaa asubuhi tarehe 04.07.2025
Mathayo 5:33-41
33 Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;
34 lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;
35 wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.
36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.
37 Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.
38 Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;
39 Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.
40 Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia.
41 Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.
Wito wa kuingia Ufalme wa Mungu;
Asubuhi ya leo tunaendelea kusoma sehemu ya hotuba ya Yesu mlimani. Leo tunasoma Yesu akifundisha juu ya kutoapa. Hapa Yesu alikuwa anafundisha kuwa wakweli na siyo kuwa waongo. Kutoishi kiapo ni kuwa muongo, ndiyo maana Yesu anasema Ndiyo iwe ndiyo, Siyo iwe siyo.
Yesu anaendelea kufundisha juu ya kutoshindana na mtu mwovu. Yesu anasema akupigaye shavu la kuume mgeuzie na la pili. Sasa ukitafsiri kupigwa shavu utapigwa kweli na utaumia. Yesu alimaanisha tusishindane na waovu, wasioamini, bali katika yote tumche yeye. Yaani Yesu anatufundisha tusiache kumwamini na kuzifuata imani nyingine zisizofaa. Anatoa mifano zaidi, kwamba atwaaye kanzu mpe na joho pia, akulazimishaye kwenda maili moja, nenda naye mbili.
Ujumbe wa Kristo asubuhi ya leo ni kumuishia yeye katikati ya changamoto nyingi maishani. Vishawishi, matatizo, malengo yasiyofikiwa n.k visitutoe kwa Kristo, maana hiyo ndiyo njia sahihi ya kuingia katika Ufalme wa Mungu. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa