Hii ni Epifania
Jumanne asubuhi tarehe 04.02.2025
1 Samweli 12:8-11
8 Yakobo alipokuwa ameingia Misri, na baba zenu walipomlilia Bwana, ndipo Bwana akawapeleka Musa na Haruni, nao wakawatoa baba zenu kutoka Misri, wakawakalisha mahali hapa.
9 Lakini wakamsahau Bwana, Mungu wao, naye akawauza na kuwatia katika mikono ya Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori, na katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya mfalme wa Moabu, nao wakapigana nao.
10 Nao wakamlilia Bwana, wakasema, Tumefanya dhambi, kwa kuwa tumemwacha Bwana, na kuwatumikia Mabaali na Maashtorethi; lakini sasa utuokoe na mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia wewe.
11 Bwana akawatuma Yerubaali, na Baraka, na Yeftha, na Samweli, akawaokoa ninyi na mikono ya adui zenu pande zote, nanyi mkakaa salama.
Mungu ni mlinzi wetu;
Baada ya Sauli kuwa ametawazwa kuwa Mfalme, Samweli sasa amezeeka na anatoa hotuba ya kuaga. Somo la asubuhi hii ni sehemu ya hotuba ya Samweli, akiwausia Taifa la Mungu kumcha Bwana daima. Anawakumbusha jinsi baba zao walivyokuwa utumwani Misri, Bwana akawatoa huko. Pamoja na baba zao kumsahau na kumuacha Bwana, Samweli anasema Bwana hakuwaacha, aliwaokoa toka mikono ya adui zao.
Samweli anawakumbusha watu walivyookolewa na Bwana katikati ya utumwa na maadui. Itukumbushe tulivyookolewa na Bwana kwa njia ya kifo cha Yesu Kristo msalabani na kufufuka. Kumbe ni Yesu Kristo pekee aokoaye, ndiye mlinzi wetu. Tuutegemee ulinzi wake ili tuwe na mwisho mwema. Amina
Jumanne njema
Heri Buberwa