Date: 
18-01-2025
Reading: 
Warumi 10:16-18

Hii ni Epifania 

Jumamosi asubuhi tarehe 18.01.2025

Warumi 10:16-18

16 Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu?

17 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.

18 Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.

Wabatizwao ni warithi wa uzima wa milele;

Mtume Paulo anaandika juu ya kuamini, kwamba imani huja kwa kusikia. Anamrejea Isaya aliyeandika juu ya watu ambao hawakuusikia ujumbe wa Mungu;

Isaya 41:26

Ni nani aliyeihubiri habari tokea mwanzo, tupate kuijua? Na tokea zamani, tupate kusema, Yeye ni mwenye haki? Naam, hapana hata mmoja aliyetujulisha; naam, hapana hata mmoja aliyetuonyesha; naam, hapana hata mmoja aliyesikia maneno yenu.

Ujumbe wa Paulo ni kulisikia neno la Mungu na kulitii. Neno la Mungu likikaa mioyoni mwetu tunaongozwa na Mungu mwenyewe. Mwenendo wetu na maisha yetu kwa ujumla humtegemea Kristo. Sisi kama waamini tuliobatizwa tunakumbushwa kuishi kwa njia ya neno la Mungu. Tusome, tutafakari, tusikilize na kujifunza neno la Mungu, tukilifanyia kazi kama Yakobo anavyoandika;

Yakobo 1:22-24

22 Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.
23 Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.
24 Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.

Tumsikie Kristo kwa njia ya neno lake ili tuurithi uzima wa milele. Amina

Uwe na Jumamosi njema

Heri Buberwa