Date:
25-10-2024
Reading:
Luka 10:17-20
Ijumaa asubuhi tarehe 25.10.2024
Luka 10:17-20
17 Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.
18 Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.
19 Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.
20 Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.
Tuishindanie Imani katika Kristo Yesu;
Injili ya Luka sura ya kumi inaanza kwa kuonesha Yesu akiwatuma wale sabini kuhubiri. Anawatuma katika makundi ya watu wawili wawili kwenda kila sehemu katika mji kupeleka habari zake. Walienda kupeleka habari za Yesu, wakarudi wakifurahi mbele ya Yesu kwamba hata pepo waliwatii kwa jina lake (Yesu)
Huenda wale sabini walisubiri pongezi kwa sababu ya kufukuza pepo kwa jina la Yesu. Yesu anawaambia wasifurahi kwa sababu pepo wanawatii, bali kwa kuwa majina yao yameandikwa mbinguni. Majina yetu yanaandikwa mbinguni kwa kumwamini Yesu, siyo kwa kufukuza pepo. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa