Date:
30-10-2023
Reading:
Mambo ya walawi 26:1-2
Jumatatu asubuhi tarehe 30.10.2023
Mambo ya Walawi 26:1-2
1 Msifanye sanamu yo yote, wala msijisimamishie sanamu ya kuchonga, wala mnara, wala msiweke jiwe lo lote lililochorwa katika nchi yenu ili kulisujudia; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
2 Zishikeni Sabato zangu, na kupastahi patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana.
Tutengeneze mambo yaliyoharibika;
Juma hili tunaelekezwa kutafakari juu ya Matengenezo ya Kanisa. Somo la asubuhi ya leo ni sehemu ya maelekezo ya Mungu kwa wana wa Israeli, pale alipowapa amri zake. Somo linataja chache tu, yaani kutoabudu sanamu na kuishika sabato ambayo baada ya kufa na kufufuka kwa Yesu ni siku ya Bwana.
Katika kitabu cha Mambo ya Walawi zinatajwa amri hizo chache, lakini upo mkazo wa kushika amri zote;
Mambo ya Walawi 26:3-4
3 Kama mkienda katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyafanya; 4 ndipo nitazinyesha mvua zenu kwa nyakati zake, na nchi itazaa maongeo yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake.Amri za Mungu zimegawanyika katika makundi mawili, zipo za wakristo na Mungu (Mimi ni Bwana Mungu wako, usijifanyie sanamu, Usilitaje bure jina la Bwana, Ikumbuke siku ya Bwana)
Pia zipo za wakristo wao kwa wao (Usiibe, usishuhudie uongo, usiue n.k)
Msingi wa amri zote hizi ni upendo, na ndiyo maana Yesu alisema amri kuu ni upendo;
Mathayo 22:36-40
36 Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? 37 Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. 40 Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.Asubuhi ya leo tunakumbushwa kuzishika amri za Bwana, tukimtazama Kristo aliye Mwokozi wetu. Tuombe atujalie upendo, ili tuishi katika utengemano wa kweli tukiwa na ushuhuda. Tutengeneze maisha yetu, maana Bwana yu karibu. Amina.
Heri Buberwa