Jumanne asubuhi tarehe 24.10.2023
Mwanzo 12:1-9
1 Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;
2 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;
3 nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.
4 Basi Abramu akaenda, kama Bwana alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.
5 Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani.
6 Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo.
7 Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea.
8 Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea Bwana madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana.
9 Naye Abramu akasafiri, akazidi kwenda pande za kusini.
Tuheshimu wito tuliopewa na Mungu;
Abramu (baadaye Abrahamu) anaambiwa atoke katika nchi yake na kwenda kwenye nchi atakayoonyeshwa na Bwana. Siyo jambo rahisi. Yaani unaambiwa uhame katika nchi ambayo ni asili yako, nchi ambayo historia ya ukoo wako iko hapo! Abramu aliondoka kama alivyoamriwa na Bwana kuelekea Kanaani, nchi ambayo Bwana aliahidi kumpa na uzao wake ambao utakuwa mkubwa.
Kuondoka kwa Abramu toka kwenye nchi ya asili yake kwenda nchi nyingine lilikuwa tendo la imani. Abramu aliheshimu wito aliopewa na Mungu, akahama Harani kuelekea Kanaani.
Sisi leo tunaitwa kumwamini na kumtumikia Yesu katika maisha yetu. Tuheshimu wito huu ili tuwe na mwisho mwema. Amina.
Siku njema.
Heri Buberwa