Jumanne asubuhi tarehe 13.06.2023
Kumbukumbu la Torati 13:6-11
6 Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako;
7 katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia;
8 usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche;
9 mwue kweli; mkono wako na uwe wa kwanza juu yake katika kumwua, na baadaye mikono ya watu wote.
10 Nawe mtupie mawe hata afe; kwa kuwa alitaka kukupotoa na Bwana, Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.
11 Na Israeli wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako.
Mungu au Ulimwengu;
Ni ujumbe toka kwa Mungu kwenda kwa taifa lake Israeli akiwaambia juu ya kumwabudu Mungu wa kweli. Mstari wa 6 tunasoma Israeli wakielekezwa kukataa ushawishi wowote ambao ungesababisha waabudu miungu mingine. Mstari wa 8 unakazia ukielekeza kuwa Israeli wasikubali wala kusikiliza habari ya kuabudu miungu mingine. Wanaelekezwa kumwabudu Mungu wa kweli.
Nasi asubuhi ya leo tunakumbushwa kumwabudu Mungu wa kweli. Ni Mungu muumbaji wetu, ambaye ametuokoa kwa njia ya kifo cha Yesu Kristo msalabani. Nguvu yake kwa njia ya Roho Mtakatifu hutuwezesha hata sasa. Tukimwamini Yesu tunakuwa tumechagua kumwabudu Mungu wa kweli, na siyo Ulimwengu. Amina.
Jumanne njema.
Heri Buberwa
Mlutheri