Date: 
08-06-2023
Reading: 
Waefeso 1:1-9

Alhamisi asubuhi tarehe 08.06.2023

Waefeso 1:1-9

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu walioko [Efeso] wanaomwamini Kristo Yesu.

2 Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

3 Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;

4 kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.

5 Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.

6 Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.

7 Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.

8 Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi;

9 akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo.

Mungu mmoja; Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Somo la asubuhi hii ni salamu ya Mtume Paulo kwa Waefeso mwanzoni mwa waraka wake kwao, ambapo anawatakia neema itokayo kwa Mungu. Katika mstari wa tatu, Mtume Paulo anamtukuza Mungu ambaye katika Utatu Mtakatifu huwapa watu wake baraka za rohoni. Paulo anamtambulisha Yesu kwa waefeso kama Mwokozi aliyewachagua ili wawe wana wake, akawakomboa kwa kuwapa msamaha wa dhambi. 

Ujumbe wa Paulo kwa waefeso katika utangulizi wa waraka ni neema ya Mungu katika kuwaokoa, akiwapa baraka zake katika Utatu Mtakatifu. Tukumbuke kuwa nasi tumekombolewa kwa neema ya Mungu kwa njia ya kifo cha Yesu msalabani. Tuliumbwa tulivyo, tumeokolewa kwa neema, na Roho Mtakatifu hutuongoza daima. Tudumu katika imani hii, kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Amina.

Nakutakia Alhamisi njema.

Heri Buberwa