Alhamisi asubuhi tarehe 01.09.2022
Luka 18:9-14
[9]Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.
[10]Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.
[11]Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
[12]Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.
[13]Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.
[14]Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.
Iweni wanyenyekevu;
Ni mfano wa watu wawili waliopanda hekaluni kusali. Farisayo akaanza kujitapa alivyo msafi, anatoa zaka, anafunga, tena akisema kabisa kuwa yeye siyo kama mtoza ushuru. Lakini mtoza ushuru yeye alifanya toba mbele za Mungu akiomba msamaha wa dhambi, na Yesu anasema huyu alienda nyumbani kwake akiwa amesamehewa.
Farisayo aliingia hekaluni akaanza kujitapa. Kiburi!
Lakini mtoza ushuru aliomba msamaha wa dhambi. Alikiri kuwa yeye ni mwenye dhambi. Unyenyekevu!
Kumbe tukimwendea Bwana kwa unyenyekevu tunasamehewa dhambi zetu. Acha kiburi, kuwa mnyenyekevu.
Siku njema.