KWAYA KUU YA KANISA KUU AZANIA FRONT YAFANYA SAFARI YA KIUINJILISTI USHARIKA WA KANISA KUU IRINGA – APRIL 2016
Kwaya Kuu ya Kanisa Kuu la Azania Front ilifanya safari ya kiuinjilisti katika Kanisa Kuu la Iringa Mjini toka tarehe 11.4.2019 hadi 14.4.2019, wakiwa wageni wa Kwaya Kuu ya Usharika huo. Kwaya hiyo iliongozwa na Baba Dean wa Kanisa Kuu la Azania Front Mch. Chediel Lwiza. Kwaya ilishiriki pia katika Ibada za kumwingiza kazini Msaidizi wa Askofu Mch.Askali Mgeyekwa.
Kwaya ilipata mapokezi makubwa kutoka Uongozi wa Dayosisi pamoja na Kwaya zote za Usharika huo. Kwaya ilipokelewa nje kidogo ya mji wa Iringa sehemu ya Ipogoro kwa shangwe kubwa. Ilikuwa ni Baraka na furaha kubwa sana.
Kwaya ilipata nafasi ya kutembelea Ofisi Kuu ya Dayosisi ambako mwanakwaya mwenzetu Mama Erica Ernest Byabato alipata nafasi ya kutoa neno katika Ibada ya asubuhi. Katibu Mkuu wa Dayosisi Ndugu Neyman Chavalla alielezea historia ya Dayosisi na kuelezea pia mpango mkakati wa Dayosisi na miradi mbalimbali kama uoteshaji na utawanyaji wa mbegu za miti ya mbao ( Pine ) na maparachichi (Avocado). Baba Askofu Blastone Gaville naye kama Mkuu wa Dayosisi alishukuru sana kwa Kwaya toka Kanisa kongwe Tanzania kutembelea Iringa. Alisema wanathamini sana utumishi wa Kanisa Kuu Azania Front kama mama wa Makanisa yote na kwa kutunza Ulutheri.
Kwaya pia ilitembelea Kituo cha Radio cha Kanisa Furaha FM na kuelezwa jinsi vipindi vinavyotengenezwa na kurushwa hewani. Jambo la kufurahisha ni Mkuu wa Kituo hicho ni mwanafunzi aliyesoma Chuo Kikuu cha Kanisa Iringa (zamani Tawi la Chuo Kikuu cha Tumaini)
Kwaya pia ilitembelea Chuo Kikuu cha Iringa na kufurahishwa sana na kozi mpya ya Ujasiriamali inayomuandaa mwanafunzi kujitegemea badala ya kufikiria habari za kuajiriwa. Kozi hiyo inatolewa kwa sasa na Chuo hicho tu.
Kwaya pia ilitembelea Kituo cha “ Huruma Diaconic Centre” ambacho kinatoa huduma kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu pamoja na wale waliofanyiwa ukatili wa kijinsia. Kwa kweli inasikitisha jinsi watoto wanavyofanyiwa vitendo vibaya na ndugu na hata wazazi kisha kuwatishia maisha Si mambo ya kuandika hapa lakini inauma sana. Kwaya ilipongeza sana Dayosisi ya Iringa kwa kuja na wazo la kuwa na Kituo hicho. Kwaya ilitoa zawadi mbalimbali kama sabuni, nguo, sukari, fedha nk.
Kwaya pia ilitembelea na kuwa na mazungumzo na Mch. Mbogo wa Kanisa Kuu Iringa na timu yake. Mchungaji alielezea kuhusu ujenzi unaoendelea wa jengo la kitega uchumi ambapo Mwenyekiti wa Kwaya Ndugu Elisha Mushumbusi alimkabidhi fedha taslimu Tsh. 500,000 kama mchango wa Kwaya.
Kwaya Kuu pia ilifanya Mkutano wake Mkuu wa Mwaka ambako mambo mbalimbali yalizungumzwa kuhusu maendeleo ya Kwaya na mwishoni walifanya zoezi la kupeana zawadi. Kila mwanakwaya alikuwa na rafiki ambaye hajui kama ni nani atampa zawadi. Ulikuwa ni mchezo mzuri sana wa kufurahisha na wenye kujenga upendo kwa kila mmoja.
Jumamosi na Jumapili Kwaya ilihudhuria Ibada ya Kumwingiza kazini Msaidizi wa Askofu Mch Askali Mgeyekwa.
Kwaya inashukuru sana uongozi wa Dayosisi ya Iringa, Kanisa Kuu na Kwaya Kuu kwa mapokezi mazuri. Pia iliweza kuacha alama ya upendo kwa kuwazawadia picha ya Kanisa kuu la Azania front.