Siku ya Jumapili, tarehe 24/10/2021, Usharika wa KKKT Kanisa Kuu Azaniafront Cathedral umefanya maadhimisho ya sikukuu ya mavuno, sikukuu ambayo hufanyika kila mwaka ili kutoa fursa kwa washarika kumtolea Mungu sehemu ya matunda au mavuno ya kazi wanazozifanya.
Ibada ya kusherehekea sikukuu hii ya mavuno kwa mwaka 2021 imefanyika katika viwanja vya usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront huku ikihudhuiriwa na washarika waliojitokeza kwa wingi wakiwa na mavuno yao tayari kwa kumtolea Mungu.
Ibada hiyo imeongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Bukoba, Dk. Aberdnego Keshomshahara, akisaidiana na Dean Chediel Lwiza, Mchungaji Charles Mzinga pamoja na Mchungaji Joseph Mlaki.
Katika Picha: Kutoka kushoto; Baba Askofu Dk. Aberdnego Keshomshahara, Mchungaji Charles Mzinga, Dean Chediel Lwiza, Mchungaji Joseph Mlaki.
Akizungumza wakati wa Ibada hiyo, Baba Askofu Dk. Aberdnego aliwapongeza washarika wa Azaniafront kwa kujitokeza kwa wingi kuhudhuria ibada hiyo huku akisisitiza umuhimu wa sikukuu ya mavuno katika maisha ya kikristo.
“Utoaji wa sadaka, mavuno, fungu la kumi n.k. huwa ni mgumu kwa walio wengi na inabidi uwe na neema ya kutoa bila mashaka, bila kinyongo na bila wasiwasi ili kunufaika na utoaji wako. Ndugu zangu, utoaji wa sadaka, mavuno au michango mingine yoyote ya kanisa unahitaji tujitoe sisi kabla ya kutoa hizo sadaka. Tujitoe sisi wenyewe tuwe sadaka kwanza kabla ya kutoa sadaka zenyewe. Hii itatusaidia kutoa kwa furaha bila manunguniko,” amesema Baba Askofu.
“Utoaji wa sadaka au mavuno ni aina ya kuwasilisha maombi yetu mbele za Mungu lakini pia utoaji wa sadaka ni sehemu ya kutoa shukrani zetu kwa Mungu juu ya neema na baraka anazotujalia kila kukicha,” ameongeza.
Kwaya ya Ukombozi kutoka Usharika wa Msasani, Dar es Salaam
Sehemu ya washarika waliohudhuria wakifuatilia ibada
Ibada ya sikukuu ya mavuno katika Usharika wa Azaniafront imehudhuriwa na washarika na vikundi vyote vya usharika. Ibada ilitanguliwa na maandamano mafupi na utoaji wa sadaka pamoja na mavuno yenyewe huku ikihitimishwa kwa mahubiri kutoka kwa Baba Askofu Dk. Aberdnego na mwisho kabisa ukifanyika mnada wa bidhaa au mavuno yaliyokuwa yamewasilishwa na washarika.
Pia Kwaya ya Ukombozi kutoka Usharika wa Msasani iliungana na Kwaya za Usharika wa Azaniafront katika kuipamba ibada hiyo kupitia tungo mbalimbali za kumtukuza Bwana wetu.
Angalia Picha: Ibada ya Mavuno 2021
Tazama AZFTV: Ibada ya Mavuno 2021
........................................................................................................................................
Habari hii imeandaliwa na; Paulin Paul/Cuthbert Swai