Date:
04-01-2022
Reading:
1 Wakorintho 1:19-22
Jumanne asubuhi tarehe 04.01.2021
2 Wakorintho 1:19-22
19 Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, yaani, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na siyo; bali katika yeye ni Ndiyo.
20 Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi.
21 Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu,
22 naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu.
Waliomngojea Mwokozi wamuona;
Mtume Paulo anawaandikia waKorintho juu ya Mungu wanayemwamini kuwa katika yeye, yote ni Ndiyo, na ahadi zake ni Ndiyo. Anawasihi wadumu katika Bwana ili wawe imara. Ukiendelea kusoma unaona Paulo akiwasifu kwa kusimama katika imani, akiwasihi wakae hivyo hivyo.
Ujumbe wa Mtume Paulo ni kama somo la waraka tulilosoma ibadani siku ya mwaka mpya, siku tatu zilizopita;
Waebrania 13:8 Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.Yesu Kristo habadiliki. Ni yule yule tangu mwanzo, leo na siku zote. Ahadi zake ni kweli. Yeye ndiye mwokozi. Ndipo katika somo la leo asubuhi, Mtume Paulo anasema "....katika yeye ni Ndiyo".
Kwa maana hiyo, tukikaa kwa Yesu, nasi mambo yetu yanakuwa Ndiyo, na mwisho wetu utakuwa Ndiyo. Yaani ahadi zake zitatimia kwetu, na tutaurithi uzima wa milele.
Tuendelee kumngoja, tutamuona.
Siku njema.