Event Date: 
29-05-2019

ZIARA YA KWAYA YA UPENDO NCHINI NAMIBIA – MAY 2019

Kwaya ya Upendo ya kanisa kuu Azania Front ilifanya ziara ya uinjilisti nchini Namibia kuanzia tarehe 3 May hadi tarehe 13 May 2019 ambapo iliongozana na Msaidizi wa Askofu Chediel Lwiza (Mkuu wa Msafara) na Chaplain Charles Mzinga. Ziara hii ilikuwa ni mualiko wa kwaya ya Tollite Hostias ya nchini Namibia ambayo inafanya shughuli zake chini ya mwamvuli wa Tuudila Mucical Works. Mualiko huu unafuatia makubaliano ya kushirikiana (MoU) kati ya kwaya hizo mbili yaliyofanyika May 2018 Usharikani Azania Front wakati Tollite Hostias Choir walipozuru Tanzania.

Kwaya ya Upendo iliwasili katika uwanja wa ndege wa Hosea Kutako jijini Windhoek saa saba mchana siku ya Ijuma tarehe 3May 2019, na kupokelewa kwa shangwe na ukarimu mkubwa na wenyeji wao Kwaya ya Tollite Hostias.

Siku ya jumamosi tarehe 4 May kwaya ya Upendo ilishiriki katika Tamasha la uimbaji lililofanyika katika usharika wa Emmanuel jijini Windhoek ambapo takriban kwaya kumi (10) zilishiriki tamasha hilo.

Siku ya Jumapili tarehe 5 May kwaya ya Upendo ilishiriki ibada katika Usharika wa Emmanuel ambapo pia Msaidizi wa Askofu Chediel Lwiza na Chaplain Charles Mzinga walishiriki kuongoza ibada na pia kutoa huduma ya Sakramenti ya Meza ya Bwana.

Jumatatu tarehe 6 kwaya ya Upendo ilishiriki tamasha jingine katika jiji la Walvis Bay na pia walipata nafasi ya kurekodi video katika jangwa na pia fukwe za za kitalii za Walvis Bay. Video hizo ni kwa ajili ya album yao mpya inayotegemewa kuzinduliwa hivi karibuni.

Jumanne tarehe 7 kwaya ya Upendo iliekea kaskazini mwa Namibia ambapo walishiriki matamasha mbalimbali na kutembelea Makao makuu ya Dayosis za Kaskazini na Magharibi. Pia walitembelea sharika za Ongenga, Nakayale, Ewaneno, Eenahna, Gloria Dei, na Omundudu.

Kwaya ya Upendo iliondoka Namibia siku ya Jumatatu tarehe 13 May 2019 na kuwasili Dar es Salaam alfajiri ya tarehe 14 May 2019.

Kwaya ya Upendo imeuona mkono wa Bwana kwenye safari hii kuanzia maandalizi mpaka wakati wa safari yenyewe na Kwaya inamshukuru Mungu sana.

Aidha kwaya inawashukuru washarika mmoja mmoja kwa kujitoa kwao kuwapeleka Namibia. Mungu awabariki sana.

Mwisho kabisa kwaya inamshukuru Msaidizi wa Askofu kwa kukubali kuongozana na Kwaya na pia Chaplain Mzinga ambao wote kwa pamoja walituongoza vizuri sana. Mungu awabariki sana.