Date: 
12-07-2025
Reading: 
Zaburi 119:57-64

Jumamosi asubuhi tarehe 12.07.2025

Zaburi 119:57-64

57 Bwana ndiye aliye fungu langu, Nimesema kwamba nitayatii maneno yake.

58 Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako.

59 Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako.

60 Nalifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako.

61 Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako.

62 Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki.

63 Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako.

64 Bwana, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako.

Msingi wa uongozi bora;

Kijana Mkristo ni chachu ya maendeleo;

Katika Zaburi hii ndefu ya 119, Daudi huwa anaimba juu ya Utukufu wa sheria ya Mungu. Katika sehemu ya tafakari ya asubuhi hii, Daudi anatambua na kukiri kwamba Bwana ndiye fungu lake na anaahidi kuyatii maagizo yake. Daudi anaomba toba na kumrejea Mungu akimuomba asimuache. Anaendelea kuahidi kuishika sheria ya Bwana na kumshukuru siku zote kwa sababu hukumu zake ni za haki. Daudi anaona dunia yote imejaa fadhili za Bwana.

Somo la leo asubuhi ni sifa kwa Mwenyezi Mungu. Daudi anamsifu Mungu, anampa utukufu. Ni wito kwetu nasi kumsifu Mungu kwa sababu ya ukuu wake na fadhili zake kwetu. Kumsifu Mungu ni zaidi ya kuimba. Yaani kwa mfano;

-Kama wewe ni baba halafu huitunzi familia yako inavyotakiwa haumsifu Mungu

-Kama hulipi madeni bila sababu haumsifu Mungu

-Mwanafunzi ambaye hasomi kwa bidii anakuwa hajamsifu Mungu 

-Kijana usiyeheshimu wakubwa hiyo siyo sifa kwa Mungu 

-Kutofuata taratibu za kazi siyo sifa kwa Mungu 

-Kuendesha bila kufuata sheria za barabarani siyo sifa kwa Mungu 

-Usipoimba kwa akili hujamsifu Mungu n.k

Kumsifu Mungu ni zaidi ya kuimba. Ni kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wetu, tukitenda kwa kadri ya neno lake. Tukitimiza wajibu na kutenda haki tunamsifu Mungu na kutangaza Ufalme wake, maana maisha yetu ni mahubiri kamili. Amina

Jumamosi njema

Heri Buberwa