Jumanne asubuhi tarehe 09.07.2024
Mhubiri 12:1-2
1 Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.
2 Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;
Bidii ya kijana, mafanikio ya Kanisa;
Ni nasaha za Mfalme Suleimani zinaendelea tena asubuhi hii kuhusu vijana. Ujumbe unasema na kijana kumkumbuka muumba wake siku za ujana wake kabla hazijaja siku zilizo mbaya, kabla haujaja wakati wa kutokuwa na furaha. Suleimani anasisitiza kumkumbuka muumba kabla ya nuru, nyota na mwezi havijatiwa giza.
Ujumbe tunaoupata asubuhi ya leo ni kutenda kazi kwa wakati. Tunaalikwa kutimiza wajibu wetu kwa wakati tukitimiza malengo yaliyokusudiwa. Kwa maana nyingine tuache uvivu maana tukiwa wavivu hatuwezi kufikia malengo. Wokovu ni sasa, na katika wokovu huo timiza wajibu wako ipasavyo wakati wote. Amina.
Jumanne njema.
Heri Buberwa