Date: 
04-07-2024
Reading: 
Kutoka 23:24-32

Alhamisi asubuhi tarehe 04.07.2024

Kutoka 23:24-32

24 Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande.

25 Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako.

26 Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.

27 Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao.

28 Nami nitapeleka mavu mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako.

29 Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua.

30 Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi.

31 Nami nitakuwekea mpaka wako tangu Bahari ya Shamu hata bahari ya Wafilisti, tena tangu jangwani hata huo Mto; kwa kuwa nitawatia wenyeji wa nchi mkononi mwako; nawe utawafukuza mbele yako.

32 Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao.

Ninyi ni barua ya Kristo;

Wana wa Israeli wako njiani kuelekea nchi ya ahadi. Walipofika Sinai Musa akapewa maelekezo na Bwana, jinsi ambavyo Israeli wangeishi kwa kumfuata. Zinaanza amri za Mungu kuanzia sura ya 20, ujumbe ambao unaendelea kwenye somo tulilosoma. Israeli wanaaswa kutoabudu miungu na kumtumikia Mungu pekee.

Ujumbe muhimu kwa Israeli ulikuwa ni kuiacha miungu na kumcha Bwana pekee. Ndiyo ujumbe unaodumu hata sasa, kwamba tumwabudu Mungu pekee. Kumwabudu Mungu ni kumwamini Yesu na kutenda yote kwa kadri ya neno lake, na kwa njia hii tunakuwa mashuhuda wa Injili maana sisi ni barua ya Kristo. Amina

Alhamisi njema

Heri Buberwa