Date: 
15-11-2022
Reading: 
Yeremia 45:1-5

Jumanne asubuhi tarehe 15.11.2022

Yeremia 45:1-5

[1]Neno hili ndilo ambalo Yeremia, nabii, alimwambia Baruku, mwana wa Neria, alipoyaandika maneno haya katika kitabu kwa kinywa cha Yeremia, mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kusema,

[2]BWANA, Mungu wa Israeli, akuambia wewe Ee Baruku;

[3]Ulisema, Ole wangu! Kwa maana BWANA ameongeza huzuni pamoja na maumivu yangu. Nimechoka kwa ajili ya kuugua kwangu, wala sioni raha.

[4]Basi, mwambie hivi, BWANA asema hivi, Tazama, niliyoyajenga nitayabomoa, na niliyoyapanda nitayang’oa; na haya yatakuwa katika nchi yote.

[5]Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema BWANA; lakini roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda.

Jiandae kwa hukumu ya mwisho;

Yeremia alitumwa kuleta ujumbe wa faraja kwa mtu aliyekata tamaa, Baruku. Mstari wa tatu unaonesha mtu mwenye huzuni na maumivu mengi, aliyechoka kwa kuugua akiwa hana raha yoyote. Bwana alitoa neno la faraja kupitia kwa nabii Yeremia akiahidi kumponya na kumtunza Baruku. 

Bwana hakuishia hapo, alimuasa kutotafuta makuu, bali kuutafuta uso wake Bwana. Bwana alisema kuwaangamiza wote wenye mwili wajitafutiao makuu. Tunakumbushwa kumtegemea Bwana, lakini kuutafuta uso wake, tayari kwa hukumu ya mwisho.

Siku njema.