Date: 
07-07-2026
Reading: 
Wakolosai 3:18-22

Jumanne asubuhi tarehe 07.07.2026

Wakolosai 3:18-22

18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana.

19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.

20 Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana.

21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

22 Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana.

Kanisa ni msingi wa malezi bora;

Mtume Paulo anawaandikia watu wa Kanisa la Kolosai yahusuyo familia, kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake. Anawaandikia wake kuwatii waume zao kama impendezavyo Bwana. Halafu anawaandikia waume kuwapenda wake zao bila kuwa na uchungu nao. Watoto wanatakiwa kuwa watii kwa wazazi wao, na watumwa kuwatii bwana zao.

Ukiangalia andiko hili la Paulo ni mawaidha yake kwa familia. Anazitaka familia kukaa kwa pamoja, kila mmoja katika familia husika akitimiza wajibu wake. Kanisa linaanzia nyumbani. Tukitimiza wajibu wetu kila mmoja, familia zetu zitastawi na Kanisa pia, hivyo Kanisa kuwa msingi wa malezi bora. Amina

Sabasaba njema.

Heri Buberwa