Date: 
03-07-2026
Reading: 
Mwanzo 45:1-15

Ijumaa asubuhi tarehe 03.07.2026;

Mwanzo 45:1-15

1 Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze.

2 Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia.

3 Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake.

4 Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri.

5 Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu.

6 Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna.

7 Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu.

8 Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri.

9 Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu, Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie.

10 Nawe utakaa katika nchi ya Gosheni, utakuwa karibu nami, wewe, na wanao, na wana wa wanao, na wanyama wako, ng'ombe zako, na yote uliyo nayo. Nami nitakulisha huko;

11 maana bado imesalia miaka mitano ya njaa; usije ukaingia katika uhitaji, wewe, na nyumba yako, na yote uliyo nayo.

12 Na tazama, macho yenu yanaona, na macho ya ndugu yangu Benyamini, ya kwamba ni kinywa changu mimi kinachosema nanyi.

13 Nanyi mtamwarifu baba yangu habari za fahari yangu yote katika Misri, na za vyote mlivyoviona; mkafanye haraka kumleta huku baba yangu.

14 Akaanguka shingoni mwa ndugu yake Benyamini, akalia; Benyamini naye akalia shingoni mwake.

15 Akawabusu ndugu zake wote, akalia nao, baada ya hayo, nduguze wakazungumza naye

Tumeitwa kutenda haki na huruma;

Yusufu alikuwa ameuzwa Misri na ndugu zake, akakaa katika nyumba ya Potifa kwa tabu sana. Lakini kwa neema ya Mungu alifikia hatua ya juu ya utawala katika Misri baada ya Farao. Njaa ilipokuwa kubwa, ndugu zake walifuata chakula Misri, Yusufu akawa mwenyeji wao. Mara ya kwanza aliwapa chakula, akawaambia wakirudi wamlete ndugu yao mdogo (Benyamini). Mara ya pili baada ya kumshawishi baba yao Yakobo, walirejea Misri kutafuta wakiwa na Benyamini.

Somo la leo linaanzia hapo, Yusufu baada ya kumuona Benyamini alilia sana. Ndipo akajitambulisha kwao, kwamba yeye ndiye Yusufu waliyemuuza. Pamoja na yote, Yusufu hakulipiza kisasi. Aliwapokea vizuri na kuwapa chakula. Mstari wa 15 ni Yusufu anawabusu ndugu zake, hii ilikuwa ni ishara ya upendo na msahama. Tupendane, tusameheane na tuhurumiane. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa