Date:
22-06-2026
Reading:
Waefeso 3:10-13
Jumatatu asubuhi tarehe 22.06.2026
Waefeso 3:10-13
10 ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho;
11 kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu.
12 Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.
13 Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu kwenu.
Pamoja tujenge Kanisa la Bwana;
Mtume Paulo anajitambulisha kama mhubiri wa Injili, aliyejitoa maisha yake kwa ajili ya Mungu. Katika utume wake huo anakiri neema ya Mungu kuwa juu yake. Ni kwa muktadha huo, tunasoma leo akiwahimiza watu wa Efeso kuishi kwa kusudi lake Kristo, yaani kumwamini, kumtegemea katika maisha ya kila siku na kumtumikia pasipo kuchoka.
Paulo anawataka wasomaji wake kujaa ujasiri, kumkaribia Bwana kwa njia ya imani. Tena anawaambia wasikate tamaa kwa jambo lolote. Ni ujumbe unaowataka kutokata tamaa katika kazi waliyoitiwa, yaani imani na utume wao kwa Mungu. Nasi katika utume wetu, tuungane kulijenga Kanisa la Bwana kwa pamoja. Amina
Uwe na wiki njema.
Heri Buberwa
Mlutheri
