Date: 
21-10-2025
Reading: 
2 Mambo ya nyakati 32:1-8

Jumanne asubuhi tarehe 21.10.2025

2 Mambo ya Nyakati 32:1-8

1 Ikawa, baada ya mambo hayo, na uaminifu huo, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akaja, akaingia katika Yuda, akafanya marago juu ya miji yenye maboma, akadhania kwamba ataipata iwe yake.

2 Basi Hezekia, alipoona ya kuwa Senakeribu amekuja, na kuazimia kupigana na Yerusalemu,

3 akafanya shauri na wakuu wake, na mashujaa wake, kuzuia maji ya chemchemi zilizokuwa nje ya mji; nao wakamsaidia.

4 Wakakusanyika watu wengi, wakazizuia chemchemi zote, na kijito kilichopita kati ya nchi, wakisema, Kwa nini, wakifika wafalme wa Ashuru, waone maji mengi?

5 Akapiga moyo konde, akaujenga ukuta wote uliobomoka, akauinua sawa na minara, na ukuta wa pili nje, akaongeza nguvu ya Milo, katika mji wa Daudi, akafanya silaha na ngao tele.

6 Akaweka maakida wa vita juu ya watu, akawakusanya kwake uwandani penye lango la mji, akawafurahisha mioyo; akisema,

7 Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye;

8 kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo Bwana, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.

Imani Iletayo ushindi;

Mfalme wa Ashuru aliyeitwa Senakeribu aliingia katika Yuda akitaka kuivamia na kuiteka. Hezekia kiongozi wa Yuda alifanya shauri na wakuu wake na mashujaa pia wakazuia mifumo ya maji kuingia katika Yuda ili waashuru wakifika wakose maji. Wakajenga kuta kuizingira Yuda ili isiwe rahisi kuivamia, akaandaa silaha za kutosha. Hezekia aliendelea kuwatia moyo watu wake akiwaambia kuwa hodari na moyo mkuu kwa sababu yupo mkuu kuliko waashuru. Hezekia aliwahakikishia watu wake kushinda kwa jina la Bwana. Wajua kilichotokea?

2 Mambo ya Nyakati 32:20-21

20 Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni.
21 Naye Bwana akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga.

Hezekia na watu wake walimlilia Bwana kwa imani, Bwana akatuma malaika aliyewaangamiza majemedari na wapiganaji wote wa Ashuru. Mfalme wa Ashuru alirudi nchini mwake kwa aibu. Alipofika watoto wake mwenyewe wakamuua kwa upanga! Yuda wakiongozwa na Hezekia walishinda vita kwa imani. Tukiwa na imani tutashinda na kuurithi uzima wa milele. Amina

Jumanne njema

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com