Date: 
18-10-2025
Reading: 
Hesabu 27:12-23

Jumamosi asubuhi tarehe 18.10.2025

Hesabu 27:12-23

12 Bwana akamwambia Musa, Panda wewe juu ya mlima huu wa Abarimu, uitazame nchi niliyowapa wana wa Israeli.

13 Na ukiisha kuiona, wewe nawe utakusanyika pamoja na baba zako, kama Haruni ndugu yako alivyokusanyika;

14 kwa sababu mliasi juu ya neno langu katika jangwa la Sini wakati wa mateto ya mkutano, wala hamkunistahi, hapo majini, mbele ya macho yao. (Maji hayo ndiyo maji ya Meriba ya Kadeshi katika jangwa la Sini.)

15 Musa akanena na Bwana akisema,

16 Bwana, Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano,

17 atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.

18 Bwana akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako;

19 kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao.

20 Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii.

21 Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za Bwana; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia.

22 Musa akafanya kama Bwana alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote;

23 kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama Bwana alivyosema kwa mkono wa Musa.

Kristo ametuweka huru;

Asubuhi ya leo tunaona Bwana akimpandisha Musa mlimani na kumuonesha nchi ya ahadi, nchi ambayo aliambiwa asingefika. Musa alitii maneno aliyoambiwa, akamsihi Bwana ampe mjumbe ambaye angewaongoza watu wake kuelekea nchi ya ahadi. Bwana akamwambia Musa kumtwaa Yoshua mwana wa Nuni na kumwekea mkono. Yaani Musa anaelekezwa kumweka "wakfu" Yoshua. Kwa hiyo tunapoweka wakfu watendakazi hatubabaishi, ni jambo la Kibiblia toka enzi. Musa alifanya kama alivyoelekezwa, akamweka Yoshua mbele ya Eleazari Kuhani na mbele ya mkutano wote. Yaani Yoshua aliingizwa kazini mbele ya usharika.

Matukio yote yanayohusu Musa kuwaongoza Israeli na Yoshua kuchukua nafasi yake yalikuwa na lengo moja, ukombozi wa wana wa Israeli kukamilika, kutoka utumwani kwenda Kanani. Mpango wa wokovu kwa wanadamu haujawahi kukoma, ndiyo maana Mungu alishuka kwa njia ya mwanawe Yesu Kristo, akafa na kufufuka kwa ajili yetu. Kwa njia ya kifo chake ametuweka huru na dhambi. Basi tudumu katika imani katika Kristo Yesu atupaye kushinda, sasa hata uzima wa milele. Amina

Jumamosi njema

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com