Date: 
08-02-2025
Reading: 
Isaya 58:8

Hii ni Epifania 

Jumamosi asubuhi tarehe 08.02.2025

Isaya 58:8

Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.

Mungu ni mlinzi wetu;

Sura ya 58 ya kitabu cha Isaya hueleza juu ya ibada ya kweli na ile ya uongo. Sura hii mara nyingi hutumika siku ya kuanza majira ya mateso, (siku ya majivu) kuwaita wakristo kuwa na maisha ya toba wakifanya ibada ya kweli. Watu hukumbushwa kufunga, kufanya matendo ya huruma, lakini zaidi kutubu na kurejea kwa Bwana.

Mistari ambayo hutumika sana siku hiyo ya majivu ni hii hapa;

Isaya 58:5-7

5 Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana?
6 Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?
7 Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?

Sasa ukisoma hapo juu unaona ni maelekezo ya kufanya ibada njema. Somo la leo ni mstari unaofuata baada ya hiyo hapo juu, kama hitimisho. Kwamba wakristo wakiwa na ibada njema, ndipo nuru yao itapambazuka kama asubuhi na afya itatokea mara, na haki itatangulia. Zaidi ya hapo wakristo wanahakikishiwa kulindwa na utukufu wa Mungu. Maisha yetu ni ibada kamili. Mungu aliye mlinzi wetu anatutaka kuwa na ibada njema, yaani kuishi maisha yanayomtukuza yeye. Uwe na Jumamosi njema. Amina

Heri Buberwa