Date: 
17-01-2025
Reading: 
Marko 1:4-8

Hii ni Epifania 

Ijumaa asubuhi tarehe 17.01.2025

Marko 1:4-8

4 Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.

5 Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.

6 Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu.

7 Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake.

8 Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.

Wabatizwao ni warithi wa uzima wa milele;

Yohana Mbatizaji alimtangulia Kristo akitangaza ujio wake kwa kuwaambia watu watubu dhambi zao na kubatizwa, tayari kwa ondoleo la dhambi. Wengi walimwendea wakabatizwa katika mto Yordani wakiziungama dhambi zao. Yohana anahubiri na kusema Yesu ajaye ana nguvu kuliko mimi (Yohana), hivyo kuonesha kwamba Yesu ajaye ndiye Mwokozi wa ulimwengu.

Yohana anasema ubatizo alioufanya yeye ulikuwa kwa maji, lakini Yesu angebatiza kwa Roho Mtakatifu. Kumbe sisi tumebatizwa kwa maji yenye neno la Mungu, katika Utatu Mtakatifu. Kwa hiyo kama Yohana alivyosema, yeye alibatiza kwa maji, bali sisi tumebatizwa kwa Roho Mtakatifu, yaani Mungu mwenyewe. Kwa kukiri ahadi ya ubatizo tumeokolewa. Dumu katika maisha hayo ya wokovu siku zote, hata uzima wa milele. Amina

Ijumaa njema

Heri Buberwa